Ticker

6/recent/ticker-posts

𝗞𝗜𝗣𝗘𝗡𝗚𝗔 𝗖𝗛𝗔𝗣𝗨𝗟𝗜𝗭𝗪𝗔 𝗞𝗨𝗪𝗔𝗦𝗜𝗟𝗜𝗦𝗛𝗔 𝗠𝗜𝗦𝗪𝗔𝗗𝗔 𝗬𝗔 𝗧𝗨𝗭𝗢 𝗬𝗔 𝗧𝗔𝗜𝗙𝗔 𝗬𝗔 𝗠𝗪𝗔𝗟𝗜𝗠𝗨 𝗡𝗬𝗘𝗥𝗘𝗥𝗘 𝗬𝗔 𝗨𝗔𝗡𝗗𝗜𝗦𝗛𝗜 𝗕𝗨𝗡𝗜𝗙𝗨


Waziri wa Elimu, Sayansi na Teknolojia, Prof. Adolf Mkenda, amesema Tuzo ya Taifa ya Mwalimu Nyerere ya Uandishi Bunifu imeendelea kuonyesha mafanikio makubwa, ambapo tangu kuanzishwa kwake Watanzania 27 wamefanikiwa kushinda katika nyanja mbalimbali ya uandishi Bunifu.

Prof. Mkenda amesema mafanikio hayo yanaonyesha namna tuzo hiyo inavyo ibua na kutambua vipaji vya waandishi bunifu nchini, huku idadi ya washiriki ikiongezeka kila mwaka kutoka ndani na nje ya Tanzania.

Amesema Serikali pia imewekeza takribani Sh. milioni 800 kwa ajili ya kuchapisha vitabu vilivyoshinda tuzo hizo na kuvisambaza katika shule za Tanzania Bara na Zanzibar, hatua inayolenga kuwafikia wasomaji wengi zaidi na kuhamasisha utamaduni wa kusoma.

Waziri Mkenda amesema tuzo hizo imeendelea kukua na kuvutia washiriki kutoka mataifa mbalimbali, jambo linaloonyesha kuongezeka kwa hadhi yake na umuhimu wa uandishi bunifu katika kukuza fasihi na lugha ya Kiswahili.

Amesema tuzo hizo pia zimekuwa jukwaa la kuwahamasisha vijana na waandishi kutumia vipaji vyao katika kutengeneza kazi zenye ubunifu na maudhui yanayoweza kuelimisha na kujenga jamii.

"Tuzo hii imeingizwa rasmi katika orodha ya tuzo za uandishi bunifu duniani, ukiitafuta mtandaoni utaona tarehe 13 April ni siku ya kutoa tuzo ya Mwalimu Nyerere ya Uandishi Bunifu" Amesema Waziri Mkenda.

Aidha, Prof Mkenda amesisitiza kuwa Serikali itaendelea kuweka mazingira wezeshi kwa ajili ya maendeleo ya uandishi bunifu na fasihi, akiwataka waandishi na wadau wa sekta hiyo kutumia fursa zinazotolewa kupitia tuzo hiyo kuendeleza vipaji vyao.



 



Post a Comment

0 Comments