Na Mwandishi wetu, Dodoma
UJENZI wa majengo matatu mapya katika Hospitali ya Jiji la Dodoma iliyopo Kata ya Nala unagharimu kiasi cha shilingi 800,000,000 mradi unaotarajiwa kuleta mapinduzi makubwa katika utoaji wa huduma za afya kwa wakazi wa jiji hilo na wilaya za jirani.
Akiwasilisha taarifa ya mradi huo mbele ya Kiongozi wa Mbio za Mwenge wa Uhuru Kitaifa mwaka 2026, Mganga Mkuu wa Jiji la Dodoma, Dr. Sebastian Pima alisema kuwa mradi huo unahusisha ujenzi wa jengo la upasuaji, wodi ya wanaume pamoja na jengo la kufulia nguo. "Utekelezaji wa mradi huu ulianza rasmi tarehe 30 Agosti 2025 baada ya kupokea fedha hizo kutoka Serikali Kuu. Hadi sasa, umefikia asilimia 97.3 na upo katika hatua ya umaliziaji (finishing), ambapo tunatarajia ukamilike rasmi tarehe 8 Juni 2026 ili uanze kutoa huduma" alisema Dr. Pima.
Aliongeza kuwa hospitali hiyo ina mkakati mkubwa wa kuhudumia wananchi wengi ambapo inatarajia kuhudumia wananchi zaidi ya 765,179 wakiwemo wanaume 373,440 na wanawake 391,739 kutoka kata zote za Jiji la Dodoma na maeneo ya pembezoni.
Nae, Kiongozi wa Mbio za Mwenge wa Uhuru Kitaifa Mwaka 2026, Wazo Mwang'onda alipongeza usimamizi thabiti wa mradi huo na kubainisha kuwa ujenzi huo unaonyesha kwa vitendo jinsi fedha za walipa kodi zinavyorudi kuwahudumia wananchi. "Tumejionea wenyewe thamani halisi ya fedha hapa Nala. Majengo haya yamejengwa kwa viwango vinavyotakiwa. Jengo la upasuaji na wodi mpya zitaenda kuokoa maisha ya wagonjwa watakaotibiwa hapa. Tunaendelea kumshukuru Rais, Dkt. Samia Suluhu Hassan kwa kujali maisha ya wananchi hasa katika miradi ya afya kama hii ambayo tunaona ina miundombinu ya kila aina.
Akitoa pongezi kwa serikali, Afisa Mtendaji wa Mtaa wa Segu Chini, Stanley Obed Msangi, alieleza kuwa kukamilika kwa majengo hayo ni ukombozi mkubwa kwa mitaa inayozunguka hospitali hiyo kwasababu itapunguza msongamano na kuongeza uhakika wa matibabu.
Mbio za Mwenge wa Uhuru Kitaifa Mwaka 2026 katika Wilaya ya Dodoma ziliweka jiwe la msingi katika mradi huo wa majengo matatu huku ukiongozwa na kaulimbiu isemayo "Tanzania ni Yetu Sote, Tushikamane kwa Pamoja Kuleta Maendeleo".
MWISHO




0 Comments