Na Mwandishi Wetu- Dodoma
Naibu Makamu Mkuu wa Chuo Kikuu cha Dodoma (UDOM) anayeshughulikia Mipango na Fedha, Profesa Jefta Sunzu, ametoa wito kwa serikali na sekta binafsi nchini kujitokeza kuunga mkono ubunifu unaofanywa na wanafunzi wa vyuo vikuu.
Profesa Sunzu ameyasema hayo Jijini Dodoma wakati akifunga maonyesho ya wiki ya tafiti na ubunifu katika chuo hicho ambapo amesema, vijana wengi ubuni mifumo ya kidijitali yenye uwezo wa kuongeza ufanisi katika uzalishaji, utoaji wa huduma na usimamizi lakini hukosa mazingira ya kuikuza na kuifikisha sokoni.
Wito huo unazilenga sekta binafsi, taasisi za umma na wadau wengine katika kuwawezesha wabunifu hao kwa kuwapatia mitaji, kuwajengea uwezo na kuwapa nafasi za kuendeleza kazi zao ili kuharakisha mabadiliko ya teknolojia ambayo ni nguzo muhimu ya kufikia malengo ya taifa yaliyoainishwa katika Dira ya Taifa ya Maendeleo 2050.
“Tuna vijana wengi wanofanya gunduzi na tafiti zenye ya kuwezesha Taifa kusonga mbele, niombe makampuni na mashirika mengine kuwasaidia kwa kuwapa mitaji, nafasi ya kutumika kwenye taasisi zao ili kulinda hazina hii,” amesema Profesa Sunzu.
Ameeleza kuwa uchumi wa kisasa unategemea zaidi ubunifu na matumizi ya teknolojia, hivyo ni muhimu kuwekeza kwa vijana wenye mawazo mapya.
Amesema changamoto iliyopo sasa ni wanafunzi hao ni kukata tamaa baada ya kumaliza masomo kutokana na kukosa msaada wa kifedha, ushauri wa kitaalamu na fursa za kuendeleza bunifu zao, licha ya kuwa wamegundua mifumo inayoweza kusaidia serikali, taasisi binafsi na jamii kwa ujumla.
Ambapo ameitaja hali hiyi kupelekea mawazo mengi yenye tija kushindwa kufikia hatua ya kutumika kuisaidia jamii na hivyo kupoteza fursa za kuchochea maendeleo ya nchi na kutanua wigo wa ukosefu wa ajira kwa vijana.
Kwa upande wake, Kaimu Mkuregenzi kutoka Kurugenzi ya tafiti machapisho na ushauri elekezi, Profesa Placidius Ndibalema amesisitiza kuwa serikali na sekta binafsi zinapaswa kuwaona vijana hao kama rasilimali muhimu ya maendeleo.
Hatua ambayo amesema zinapaswa kuwawezesha mitaji na kuwapa motisha ya kuendeleza bunifu zao hatua itakayochagiza ushindani wa Taifa katika uchumi wa kidijitali, kuimarisha utoaji wa huduma na kuchangia maendeleo ya kijamii na utekelezaji wa malengo ya Dira ya Taifa ya Maendeleo 2050.




0 Comments