Ticker

6/recent/ticker-posts

IAA YAWEKEZA TEKNOLOJIA YA KISASA! MKUFUNZI ARUSHA AFUNDISHA MWANAFUNZI DODOMA


Na Carlos Claudio, Dodoma.

Chuo cha Uhasibu Arusha (IAA) kimesema kuwa maandalizi ya mashindano ya Kombe la Mataifa ya Afrika (AFCON) 2027 ni fursa muhimu kwa taasisi za elimu nchini kujiandaa kushiriki kikamilifu katika kutangaza utalii wa Tanzania na kukuza ujuzi wa wanafunzi wanaosomea sekta hiyo.


Akizungumza na waandishi wa habari katika banda la IAA kwenye Maonesho ya Wiki ya Utumishi wa Umma yanayoendelea katika Viwanja vya Chinangali Park jijini Dodoma, Meneja wa Kampasi ya Dodoma wa IAA, Prof. Epaphra Manamba, alisema AFCON si tukio la michezo pekee bali ni jukwaa la kimataifa la kuitangaza Tanzania kwa wageni watakaofika kutoka mataifa mbalimbali.


"AFCON ni mchezo na burudani, lakini pia kwa mazingira ya nchi yetu na nafasi ya Arusha kama kitovu cha utalii, ni fursa kubwa ya kujitangaza. Tuna programu ya utalii, hivyo tunajiandaa kuwawezesha wanafunzi na walimu wetu kushiriki kikamilifu katika maeneo yanayohusiana na utalii wakati wa mashindano hayo," alisema Prof. Manamba.


Alisema kupitia mashindano hayo, wanafunzi wa IAA watapata nafasi ya kutangaza vivutio vya utalii vya Tanzania pamoja na kuonesha umahiri wao katika kuwahudumia wageni kutoka mataifa mbalimbali ambao baadhi yao hawana uelewa wa kutosha kuhusu Tanzania.


Prof. Manamba alieleza kuwa baada ya AFCON, chuo hicho kitafanya tathmini ya namna programu yake ya utalii ilivyochangia katika maandalizi na mafanikio ya tukio hilo kubwa la bara la Afrika.


Katika hatua nyingine, Prof. Manamba alisema IAA imeendelea kuimarisha matumizi ya teknolojia katika utoaji wa elimu ili kuwafikia wanafunzi wengi zaidi bila kujali mahali walipo.


Alisema kutokana na maendeleo ya teknolojia, mwanafunzi anaweza kupata huduma za elimu kutoka IAA akiwa popote nchini mradi awe na uwezo wa kuunganishwa na mifumo ya chuo.


"Tumewafikia wanafunzi wengi ambao kwa sababu mbalimbali, ikiwemo majukumu ya kazi au ya kifamilia, wasingeweza kujiunga na masomo ya kawaida. Leo hii karibu kila tawi lina Smart Board na huduma za intaneti, hivyo mkufunzi akiwa Arusha anaweza kufundisha wanafunzi waliopo Dodoma kwa wakati mmoja," alisema.


Aidha, alisema ongezeko la watalii nchini limeongeza mahitaji ya wataalamu wa sekta hiyo, jambo ambalo limechangia kuongezeka kwa wanafunzi wanaojiunga na programu ya utalii inayotolewa na IAA.


Prof. Manamba alisisitiza kuwa chuo hicho kinaweka mkazo mkubwa katika elimu inayojenga ujuzi wa vitendo (Competence-Based Education), ili kuhakikisha wahitimu wake wanakuwa na uwezo wa kufanya kazi kwa ufanisi au kujiajiri mara baada ya kuhitimu.


Akizungumzia utekelezaji wa Dira ya Taifa ya Maendeleo 2050, alisema IAA itaendelea kuwekeza katika mitaala inayozingatia ubunifu, ujuzi na uwajibikaji jumuishi ili kuandaa wataalamu watakaosaidia kujenga uchumi shirikishi na endelevu.


"Dira ya Taifa ya 2050 imeipa sekta binafsi nafasi kubwa katika maendeleo ya nchi. Serikali itaendelea kuandaa mazingira na miundombinu bora huku sekta binafsi ikichukua nafasi yake katika kuchochea ukuaji wa uchumi," alisema.


Aliongeza kuwa IAA imeanzisha kituo cha ubunifu wa biashara (Business Incubator) kinachowasaidia wanafunzi kuendeleza mawazo yao ya biashara, kusajili kampuni, kuunganishwa na wadau mbalimbali na kupata msaada wa kitaalamu kabla hata ya kuhitimu masomo yao.


Kwa upande wake, mhitimu wa IAA ngazi ya Shahada na Shahada ya Uzamili, Justine Kitaja, alisema anajivunia kuwa sehemu ya mafanikio ya chuo hicho na kukipongeza kwa kuandaa mitaala inayozingatia mahitaji halisi ya soko la ajira.


Akiwa balozi wa IAA, Kitaja aliwahamasisha vijana kutumia fursa zilizopo chuoni hapo, akisema elimu inayotolewa inawajengea uwezo wa kujiajiri, kuajiri wengine na kutoa mchango mkubwa katika maendeleo ya taifa.

Post a Comment

0 Comments