Jamii imetakiwa kuendelea kutambua na kuthamini mchango wa baba katika familia kwa kuwa wao ni nguzo muhimu katika malezi ya watoto na maendeleo ya jamii.
Wito huo umetolewa leo Juni 21,2026 na Kaimu Mkurugenzi wa Mtuwa Foundation, Bi. Dorah Michael, wakati wa maadhimisho ya Siku ya Baba Duniani.
Katika kuadhimisha siku hiyo, Mtuwa Foundation ilitembelea wagonjwa katika Hospitali ya Santijema pamoja na watoto wanaolelewa katika Kituo cha watoto yatima na Wanaoishi katika Mazingira Magumu cha Rahman Orphanage Center, ambapo walitoa zawadi mbalimbali na faraja kwa makundi hayo yenye uhitaji.
Akizungumza wakati wa ziara hiyo, Dorah amesema taasisi hiyo inamshukuru Mwenyezi Mungu kwa kuwajalia fursa ya kuwafikia wahitaji na kushiriki nao maadhimisho ya Siku ya Baba Duniani kupitia matendo ya upendo na huruma.
Amesema shughuli hizo zinaendeleza maono ya marehemu Mzee Mtuwa ambaye alikuwa mstari wa mbele katika kusaidia jamii na kufanya matendo ya kiimani, huku taasisi hiyo ikiendelea kuenzi na kudumisha urithi wake kwa kuwahudumia wenye uhitaji.
Dorah ametoa wito kwa wananchi kuendelea kutembelea na kusaidia makundi yenye uhitaji katika jamii, akisisitiza kuwa kufanya hivyo kunaleta faraja kwa wahitaji na kuimarisha mshikamano wa kijamii, huku akibainisha kuwa kaulimbiu ya mwaka huu ni "Mshikamano wa Baba ni Nguvu katika Familia."

0 Comments