Wakenya wameonesha kusikitishwa na matukio ya uharibifu wa rasilimali na mali za umma na za binafsi Nchini humo, wakisisitiza kusimama kidete na Rais wa Tanzania Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan kutokana na kauli yake ya kutaka udhibiti mkali kwa wote wanaohamasisha na kuratibu matukio ya uvunjifu wa amani Nchini.
"Hapa Kenya tupo na sheria zetu, Tanzania wana sheria zao na Uganda wanazo sheria zao. Kila Nchi ina sheria na serikali yake lakini nataka kusema kwamba Wakenya tumezoea vibaya, kuchoma nchi yetu, kuvunja maduka, kuiba na kufanya maovu."
"Tusifikiri Tanzania ni Kenya, Mimi nitasimama na Mama Samia Suluhu Hassan na hata ukimuona anajibu Wakenya ni kwasababu tuna tabia moja Kenya imetushinda tunahamia Nchi nyingine." Amesema Aron Owiti, Raia wa Nairobi Nchini Kenya.
Vurugu na maandamano ya sasa nchini Kenya yanatokana hasa na hasira za wananchi dhidi ya serikali kuwaruhusu wanajeshi wa Marekani kujenga kituo cha karantini ya ugonjwa wa Ebola mjini Nanyuki, kilichokusudiwa kutibu raia wa kigeni. Wananchi wanapinga vikali mpango huo wakihofia kuletewa ugonjwa huo hatari nchini mwao, na wamekasirishwa zaidi na hatua ya serikali kuendelea na ujenzi huo kinyume cha amri ya Mahakama Kuu.
Maandamano haya yamegeuka kuwa ya vurugu kubwa baada ya waandamanaji kuanza kuharibu miundombinu mbalimbali na kuvamia vitega uchumi na kuiba mali mbalimbali, jambo lililosababisha vifo vya raia kadhaa na majeraha.

0 Comments