Ticker

6/recent/ticker-posts

TANGA YAGEUKA KITOVU CHA ELIMU, UJUZI NA UBUNIFU TANZANIA

Mkoa wa Tanga umeanza kuvuta macho ya taifa baada ya kuwa mwenyeji wa Maadhimisho ya Wiki ya Elimu, Ujuzi na Ubunifu 2026, yakilenga kuonesha namna elimu na teknolojia vitakavyochangia kufanikisha Dira ya Taifa ya Maendeleo 2050.

Akizungumza na waandishi wa habari leo Agosti 17,2026 Mkuu wa Mkoa wa Tanga Balozi Dkt. Batilda Burian amesema maadhimisho hayo si tukio la kawaida, bali ni jukwaa linalowakutanisha wabunifu, watafiti, vyuo vikuu, taasisi za elimu na sekta binafsi ili kuonesha suluhisho za maendeleo kupitia maarifa.

Kaulimbiu ya mwaka huu ni “Elimu, Ujuzi na Ubunifu: Njia ya Kufikia Dira ya Taifa 2050,” ikiwaweka washiriki katika nafasi ya kuonesha mchango wa kila sekta katika safari ya maendeleo ya Tanzania.

"Zaidi ya washiriki 300 kutoka vyuo vikuu, taasisi za utafiti, vyuo vya ufundi na mashirika ya sayansi na teknolojia tayari wameweka mabanda yao hapa katika viwanja vya Shule ya Sekondari Usagara mjini Tanga kwaajili ya kuonesha kazi zao,"amesema.

Amesema maonyesho hayo yalianza Agosti 15 na yataendelea hadi Agosti 24 na kufunguliwa rasmi Agosti 18 na Waziri wa Elimu, Sayansi na Teknolojia, Profesa Adolf Mkenda.

"Mbali na kutazama bunifu mbalimbali, wananchi watapata fursa ya kujifunza teknolojia mpya, ubunifu wa wanafunzi na tafiti zinazoweza kutatua changamoto katika kilimo, afya, viwanda na mazingira,"amesema.

Kwa mara moja ndani ya wiki hii, taasisi za elimu na utafiti kutoka maeneo mbalimbali ya Tanzania zinakutana Tanga, na kufanya mkoa huo kuwa kitovu cha maarifa, ujuzi na ubunifu kwa maendeleo ya taifa.




Post a Comment

0 Comments