Wakati ajira na ujuzi vikiendelea kuwa ajenda muhimu nchini, vijana 46 kutoka taasisi mbalimbali za elimu ya ufundi na mafunzo ya ufundi stadi (TVET) wamekutana mkoani Tanga kuwania nafasi ya kuiwakilisha Tanzania katika Mashindano ya Kimataifa ya Ujuzi.

Mashindano hayo ya Taifa ya Ujuzi 2026 yameandaliwa na Baraza la Taifa la Elimu ya Ufundi na Mafunzo ya Ufundi Stadi (NACTVET) kwa kushirikiana na Wizara ya Elimu, Sayansi na Teknolojia yanafanyika katika viwanja vya Shule ya Sekondari Usagara ikiwa ni sehemu ya maadhimisho ya Wiki ya Elimu, Ujuzi na Ubunifu.

Akizungumza na vyombo vya habari leo Agosti 17,2026 mara baada ya kukagua maandalizi ya mashindano hayo Katibu Mtendaji NACTVET Dkt. Mwajuma Lingwanda amesema kuwa washiriki hao walifika hatua ya kitaifa baada ya kufuzu mashindano ya ngazi ya kanda, ambapo walishindana katika maeneo tisa ya ujuzi. 

"Sasa wanapimwa uwezo wao kwa kazi za vitendo chini ya usimamizi wa waamuzi na wataalamu wa fani mbalimbali,"amesema.

Dkt. Lingwanda amesema maandalizi ya mashindano hayo yamekamilika, huku waamuzi, washiriki na wataalamu wakiwa tayari kuhakikisha ushindani unafanyika kwa viwango vya kitaifa na kimataifa.

Washindi wa kwanza katika kila eneo la ujuzi wataibeba bendera ya Tanzania kwenye jukwaa la kimataifa, jambo linaloifanya Tanga kuwa mahali ambapo ndoto za vijana wengi zinaanza safari ya kwenda duniani.

Kwa upande wake Mkurugenzi wa Udhibiti ubora kutoka NACTVET Dkt. Jofrey Oleke amezitaja fani hizo kuwa ni upishi, uhandisi wa mitambo, uwekaji wa vigae sakafuni na ukutani, uchomeleaji na uungaji vyuma, ushonaji, ubunifu na teknolojia ya nguo, mtandao wa vitu, ufundi umeme, urembo tiba na mekatroniki.

"Malengo yetu ni kuona Tanzania inashiriki mashindano haya kikanda na pia kidunia, hii taasisi ya world skills ni mtandao mkubwa wa nchi zote duniani yenye malengo ya kukuza ujuzi duniani,"