Ticker

6/recent/ticker-posts

IGP WAMBURA AAHIDI USAWA, FURSA ZA AJIRA JESHI LA POLISI



Na Mwandishi wetu,Dar es Salaam

Mkuu wa Jeshi la Polisi nchini, IGP Camillus Wambura, amesema ni matarajio ya Jeshi hilo kuendelea kutoa fursa nyingi zaidi kwa Vijana wa Kitanzania kutoka maeneo mbalimbali ya Nchi kama sehemu ya Mkakati wake wa kuendelea kuwa taswira halisi ya Tanzania na sehemu ya matumaini kwa Vijana.

Amesema hatua hiyo pia inalenga kuleta usawa na kuondoa ubaguzi katika ajira za vyombo vya ulinzi na usalama kwa Watanzania, ikiwa pia ni dhihirisho la dhamira ya serikali ya kutoa kipaumbele kwa vijana wenye sifa bila kujali historia zao za kimaisha. 

Kwenye hafla ya kuhitimisha Mafunzo ya Maafisa na Wakaguzi Wasaidizi wa Jeshi la Polisi, kozi namba 1 ya mwaka 2025/2026, Kurasini Jijini Dar es Salaam, IGP Wambura ametolea mfano wa sehemu ya mafanikio makubwa yaliyopatikana katika mahafali yaliyofanyika kwenye shule ya Polisi Moshi, akisema jumla ya wanafunzi 5,514 wa kozi ya awali waliohitimu mafunzo katika shule hiyo na kuwa askari Polisi, miongoni mwao wakitokea katika vituo vya kulelea watoto yatima na kutoka kwenye familia duni lakini wenye sifa za kuweza kupata nafasi hiyo.

 "Wapo wenye elimu za kidato cha nne, kidato cha sita na chuo kikuu, tulihakikisha tunawafikia na wanapata ajira ndani ya Jeshi letu la Polisi na hii ni sehemu ya dhamira yako Mhe. Rais Samia Suluhu Hassan ya kuhakikisha fursa ndani ya Jeshi la Polisi zinawafikia makundi mbalimbali bila ubaguzi huku tukitoa nafasi kwa Vijana wenye sifa kulitumikia taifa lao na kujenga maisha kupitia ajira hizi."amesema IGP Wambura.

Katika hafla hiyo ambayo iliongozwa na Mgeni rasmi Rais Samia, Mkuu huyo wa polisi alitumia fursa hiyo kumhakikishia Rais wa Tanzania kuhusu uendelevu wa mpango huu mzuri, akisisitiza kuwa jeshi la Polisi litahakikisha linatekeleza hilo kwa kufuata misingi ya haki na uwazi katika chaguzi zote za ajira zitakazofuata huko mbeleni.

Post a Comment

0 Comments