JESHI la Polisi Kanda Maalumu ya Dar es Salaam limefanikiwa kupata sehemu ya kichwa cha aliyekuwa mwanafunzi wa Chuo cha Usimamizi wa Fedha (IFM), James Temba, ambaye mwili wake ulipatikana ukielea katika Mto Msimbazi kabla ya kuzikwa mkoani Kilimanjaro.
Akizungumza na waandishi wa habari jijini Dar es Salaam, Kamanda wa Polisi Kanda Maalumu ya Dar es Salaam, SACP Jumanne Muliro amesema kichwa hicho kimepatikana baada ya uchunguzi wa kina uliofanywa na Jeshi la Polisi kwa kushirikiana na vyombo vya uchunguzi wa kisayansi.
Alisema sehemu ya kichwa hicho ilikutwa katika eneo la Kitunda Kibeberu, Wilaya ya Ilala, ikiwa imefukiwa ardhini.
Muliro amesema hadi sasa watu watano wamekamatwa kuhusiana na tukio hilo, akiwemo mganga wa kienyeji anayefahamika kwa jina la Saidi Ally maarufu Side Mzigua (31).
Alisema taratibu za kisheria zinaendelea kukamilishwa ili watuhumiwa hao wafikishwe kwenye vyombo vya sheria.
Aidha, aliwashukuru wananchi pamoja na mamlaka mbalimbali za uchunguzi wa kisayansi kwa ushirikiano uliowezesha kupatikana kwa sehemu ya kichwa hicho.
Muliro alitoa wito kwa wananchi kuepuka kusambaza taarifa za upotoshaji wakati uchunguzi wa matukio ya kihalifu ukiendelea.
Alisema Jeshi la Polisi linaendelea kulaani tukio hilo la mauaji na kusisitiza kuwa linaendelea kufuatilia jalada la kesi hiyo ili watuhumiwa wachukuliwe hatua za kisheria stahiki.

0 Comments