Na Mwandishi wetu,Dar es Salaam
Mwenyekiti wa kamati ya kusukuma mchakato wa maridhiano ya Kitaifa na Mchambuzi wa masuala ya siasa Bw. Charles Odero amekishauri Chama cha demokrasia na maendeleo Chadema kukaa na kuifanyia kazi barua ya Ofisi ya msajili wa vyama vya siasa Nchini pamoja na kuomba kikao na Msajili wa vyama vya siasa Jaji Mstaafu Francis Mutungi ili kujadiliana na kuleta suluhu ya pamoja miongoni mwao.
Odero amebainisha hayo wakati akizungumza na waandishi wa habari Jijini Dar Es Salaam, ikiwa ni siku moja mara baada ya taarifa ya msajili kutoka ikieleza kukiandikia barua Chadema, ikitoa siku 13 kwa Chama hicho kueleza ni kwanini kisichukuliwe hatua za kusimamishiwa usajili wake kutokana na kuvunja sheria ya Vyama vya siasa Nchini pamoja na baadhi ya Viongozi wake kutoa kauli zenye kuhatarisha amani na usalama wa Tanzania.
"Kwa Ofisi ya msajili wa vyama vya siasa, pale kwao mlango tu unakutana na maneno, jumba la demokrasia. Maana yake pale si eneo la kushtakiana ama kuhukumiana, maana yake pale ni jumba la kulea na kutunza demokrasia. Kwahiyo kama mlezi wa vyama vya siasa, nitoe rai kwa Msajili kuwa kuna wakati ikitokea jambo kwa mwanasiasa kuvuka mipaka basi njia za mazungumzo na maridhiano iwe kipaumbele zaidi kama sehemu ya kulea demokrasia badala ya kutunushiana misuli." amekaririwa akisema Bw. Odero.
Katika barua ya Msajili wa vyama vya siasa kwa Chadema yenye kumbukumbu namba HA.322/362/16A/22 ya Mei 7, 2026, Msajili amesema ofisi yake imekuwa ikifuatilia kwa karibu mwenendo wa viongozi wa CHADEMA, kauli zao katika mikutano ya hadhara, taarifa za vikao vya chama pamoja na maudhui yanayosambazwa kupitia vyombo vya habari na mitandao ya kijamii.
Miongoni mwa hoja zilizotajwa kwa uzito mkubwa ni kauli zinazodaiwa kutolewa na Makamu Mwenyekiti wa CHADEMA Bara, John Heche, kuhusu mpango wa kuitisha maandamano nchi nzima kushinikiza kuachiwa kwa mwanasiasa wa upinzani Tundu Lissu.
Kwa mujibu wa Msajili, kauli hizo zinaweza kutafsiriwa kama kuhamasisha taharuki, kuchochea migogoro ya kisiasa pamoja na kuingilia mwenendo wa shauri ambalo bado lipo mahakamani.
Barua hiyo pia imemnukuu Mwenyekiti wa CHADEMA Wilaya ya Korogwe, Oliver Kisaka, kwa madai ya kutoa matamshi yanayohusishwa na “mageuzi makubwa” pamoja na matukio ya Oktoba 29, 2025, huku Msajili akieleza kuwa baadhi ya kauli hizo zinaweza kufasiriwa kama uchochezi au kuhamasisha matumizi ya nguvu kisiasa.

0 Comments