Na Mwandishi wetu,Dodoma
Mamlaka ya vitambulisho vya Taifa NIDA katika kipindi cha Julai 2025 hadi Aprili 2026, imesajilu na kutambua watu 1,145,334 wenye umri wa miaka 18 na kuendelea, huku jumla ya watu 857,244 wakipatiwa namba za utambulisho wa Taifa na hivyo kufanya jumla ya watu wote waliopatiwa namba hizo mpaka sasa kufikia 22,654,206.
Kulingana na Waziri wa mambo ya ndani ya Nchi Mhe. Patrobas Katambi leo Mei 25, 2026 Bungeni Mjini Dodoma wakati akiwasilisha makadirio ya mapato na matumizi ya Wizara yake kwa mwaka 2026/27, namba hizo zinawezesha wananchi kutambulika wakati wa kupata huduma mbalimbali za kiuchumi na kijamii katika Taasisi za umma na za binafsi, akihimiza pia waajiri wote nchini kuhakikisha kuwa waajiriwa wao wanahakikiwa kwa kutumia namba za NIDA ili kujiridhisha kuhusu uraia wao pamoja na taarifa nyingine za utambuzi, kama sehemu ya kuendelea kuimarisha usalama wa Tanzania.
"Pamoja na Serikali kusogeza huduma za ugawaji wa vitambulisho karibu na wananchi, na kuanzisha huduma ya kutuma ujumbe mfupi kwa wananchi ambao vitambulisho vyao vimechapishwa kuwataka kufika katika ofisi za wilaya walizojisajili na kuvichukua, bado kuna vitambulisho 668,822 katika ofisi za wilaya za NIDA ambavyo havijachukuliwa."
"NIDA pia imeanzisha namba maalum ya kutuma ujumbe mfupi bila malipo (sms) ambayo ni 15274. Namba hiyo inamuwezesha mwananchi kufuatilia hatua ya maombi ya kitambulisho cha Taifa ilipofikia pamoja na kupata namba yake ya utambulisho bila kulazimika kufika katika ofisi za NIDA. Aidha, katika kuhakikisha NIDA inakuwa na kanzidata yenye taarifa sahihi za watu, Serikali imetoa kibali maalum cha mwaka mmoja kuanzia mwezi Oktoba 2025 hadi Septemba 2026 cha kuruhusu wananchi waliotoa taarifa zisizo sahihi wakati wa usajili, kufanya mabadiliko ya taarifa hizo kwa kutoa taarifa sahihi." Amesema Waziri Katambi.
Katika hatua nyingine, Waziri Katambi amesema NIDA inaendelea kutekeleza maelekezo ya Rais Samia Suluhu Hassan ta kuhakikisha mifumo ya taasisi zinazotoa huduma kwa wananchi inasomana ambapo kwa Julai 2025 hadi Aprili 2026, NIDA imeunganisha taasisi 17 na mfumo wa usajili na utambuzi na kufanya jumla ya Taasisi 147 zilizounganishwa ndani ya mfumo huo.

0 Comments