Ticker

6/recent/ticker-posts

VIJANA TUTAMSAIDIA RAIS SAMIA KUPINGA MACHAFUKO YA NCHI




 Na Mwandishi wetu,Dar es Salaam

Vijana wametakiwa kulinda amani na kujiepusha na vitendo vinavyoweza kusababisha machafuko au kuvunja sheria, msisitizo ukitolewa kuwa utulivu wa taifa ni msingi wa ustawi na maendeleo ya kiuchumi na kijamii.


Wakizungumza na waandishi wa habari leo Jumatatu Juni 29, 2026, Mkazi wa Dar es Salaam, Vin Alex, amesema Tanzania imeendelea kujulikana kama nchi yenye amani kwa muda mrefu, hivyo kila mwananchi ana wajibu wa kushirikiana na serikali kuhakikisha hali hiyo inadumu.


"Tanzania yetu ni ya amani. Tusishiriki kwenye machafuko au matukio ya uvunjifu wa amani nchini. Serikali pia ijizatiti kuhakikisha amani inaendelea kuwepo kwa kudhibiti wavunjifu wa sheria. Sisi wananchi tupo tayari kuungana na serikali katika kulinda amani,"amesema.


Ameongeza kuwa vijana wanapaswa kuwa waangalifu dhidi ya ushawishi wowote unaoweza kuwafanya wajihusishe na vitendo visivyokubalika kisheria, akisisitiza kuwa jukumu la kulinda amani linawahusu Watanzania wote.


Kwa upande wake, Boniface Makomba, ambaye ni mlemavu na mkazi wa Dar es Salaam, amesema maandamano au machafuko yanaweza kuathiri shughuli za uzalishaji, biashara na utoaji wa huduma, hali inayoweza kudhoofisha uchumi na kuchelewesha maendeleo.


"Tusiingie kwenye mikumbo vijana. Maandamano yatavuruga amani na kudhoofisha uchumi na maendeleo yetu," amesema.


Kauli za wananchi hao zinakuja wakati ambapo Watanzania wengi bado wanakumbuka matukio yaliyotokea wakati wa Uchaguzi Mkuu wa Oktoba 29, 2025, ambapo maeneo mbalimbali nchini yalishuhudia vurugu na uharibifu wa miundombinu. Matukio hayo pia yalihusishwa na vifo vya watu, pamoja na uharibifu wa miundombinu mbalimbali.


Wananchi hao wamehimiza kila Mtanzania, hususan vijana, kuendelea kutanguliza mazungumzo, kuheshimu sheria za nchi na kushiriki katika shughuli za maendeleo kwa njia za amani ili kuendeleza utulivu na mshikamano wa taifa.

Post a Comment

0 Comments