Ticker

6/recent/ticker-posts

VIJANA WATAKIWA KUJIEPUSHA NA USHAWISHI WA KUSHIRIKI MAANDAMANO





Vijana nchini wametakiwa kujiepusha na ushawishi wa kushiriki maandamano yanayoweza kuhatarisha amani na utulivu wa nchi, huku wakihimizwa kuendelea kushiriki shughuli za uzalishaji na maendeleo badala ya vitendo vinavyoweza kusababisha athari kwa jamii na uchumi.


Akizungumza jijini Dar es Salaam leo Jumapili Juni 28, 2026, mkazi wa jiji hilo Bw. Ibrahim Ramadhan amesema licha ya kuwepo kwa ushawishi mkubwa wa kuwahamasisha wananchi kuingia kwenye maandamano, ni muhimu kutafakari kwanza athari zinazoweza kujitokeza endapo watu watakubali kushiriki. Amesema kupotea kwa amani kunaweza kuathiri shughuli za kila siku za wananchi na kudhoofisha uchumi wa nchi.


Naye Hussein Kombo, mkazi wa Ilala, amesema maandamano si njia muafaka ya kutatua changamoto zinazowakabili wananchi. Amesema maandamano yanaweza kuwa chanzo cha vurugu, hali inayowafanya wananchi kushindwa kufanya kazi zao na kuathiri maendeleo ya kijamii na kiuchumi.


Kombo amerejea matukio ya Oktoba 29, 2025, akisema vurugu zilizotokana na maandamano ya siku hiyo zilionesha athari zinazoweza kujitokeza pale amani na utulivu vinapovurugika. Amesisitiza kuwa vijana wanapaswa kutumia njia za amani na zinazozingatia sheria katika kutoa maoni yao ili kulinda mshikamano wa taifa.


Kwa upande wake, Abbas Sarongo, mkazi wa Dar es Salaam, amesema maandamano yanaweza kukwamisha shughuli za uzalishaji, biashara na usafiri, jambo linaloweza kusababisha hasara kwa wananchi na uchumi kwa ujumla. Amesema amani ndiyo msingi wa maendeleo, hivyo kila Mtanzania ana wajibu wa kuilinda na kuitunza.

Post a Comment

0 Comments