Ticker

6/recent/ticker-posts

KASI YA UKUAJI WA SEKTA YA BIASHARA NA UWEKEZAJI JIJINI DODOMA YAWAVUTIA WANAOTEMBELEA SABASABA, 2026

 



Na Mwandishi wetu, Dar es Salaam

MKUU wa Divisheni ya Biashara, Viwanda na Uwekezaji kutoka Jiji la Arusha, John Kilunge ametembelea banda la Halmashauri ya Jiji la Dodoma katika Maonesho ya 50 ya Kimataifa ya Biashara ya Sabasaba yanayoendelea jijini Dar es Salaam na kupongeza kasi ya ukuaji wa shughuli za biashara na uwekezaji ndani ya jiji hilo.


Akiwa katika banda hilo, alipata maelezo kuhusu huduma mbalimbali zinazotolewa na Halmashauri ya Jiji la Dodoma pamoja na fursa za uwekezaji zilizopo, hususan katika sekta ya ardhi, biashara na maendeleo ya miundombinu ya kiuchumi.


Akizungumza baada ya kutembelea banda hilo, Kilunge alisema kuwa Jiji la Dodoma limeendelea kuonesha mafanikio makubwa katika kukuza mazingira ya biashara na kuvutia wawekezaji kupitia mipango yake ya maendeleo na upanuzi wa huduma kwa wananchi. "Dodoma inaonesha mwelekeo mzuri wa ukuaji wa biashara na uwekezaji. Ni jiji linalokua kwa kasi na lenye fursa nyingi kwa wafanyabiashara na wawekezaji" alisema Kilunge.


Katika hatua nyingine, Afisa Biashara Jiji la Dodoma, Ruth Kingu alieleza kuwa  maonesho hayo yamekuwa jukwaa muhimu la kuutangaza uwezo wa Jiji la Dodoma katika biashara, uwekezaji na utoaji wa huduma, huku yakisaidia kujenga ushirikiano na wadau kutoka maeneo mbalimbali nchini.


Kwa upande wake, mkazi wa Kahama aliyetembelea banda hilo, Kisumu Nyamtela alisema kuwa ushiriki wa jiji hilo katika Maonesho ya Sabasaba unalenga kutangaza huduma zinazotolewa na halmashauri pamoja na fursa mbalimbali za uwekezaji zilizopo. "Ninawiwa kutembelea Dodoma kujionea kulivyobadilika, mnajitangqza vizuri sana" alisema Nyamtela.


Halmashauri ya Jiji la Dodoma inashiriki katika Maonesho ya 50 ya Kimataifa ya Biashara ya Sabasaba kwa lengo la kutangaza fursa za uwekezaji, huduma za ardhi, miradi ya maendeleo na vivutio vya kiuchumi vinavyopatikana katika jiji hilo.

Post a Comment

0 Comments