Akizungumza leo Oktoba 31,2026 katika kampeni hiyo, Afisa kutoka kikosi cha usalama barabarani mkoa wa Dodoma kitengo cha elimu SGT Ester Makalo amesisitiza kuwa watembea kwa miguu wana haki ya kutumia vivuko vya waenda kwa miguu muda wote mchana na usiku na kwamba madereva wanapaswa kuwapa nafasi wanapotaka kuvuka barabara.
Amesema kila mtumiaji wa barabara ana wajibu wa kuhakikisha usalama wake na wa wengine, akiwataka madereva kuwa makini na kuzingatia sheria za usalama barabarani.
“Familia zetu zinatusubiri nyumbani, tunataka kila mmoja wetu awe balozi wa usalama barabarani na kusaidia kujenga utamaduni wa matumizi sahihi ya barabara,” amesema.
Aidha, ametoa wito kwa watumiaji wa barabara kuwa makini katika kipindi hiki cha kuelekea mwisho wa mwaka, ambacho pia kinaambatana na matarajio ya kuwepo kwa mvua nyingi.
Amesema mabadiliko ya hali ya hewa yanaweza kuongeza hatari kwa watumiaji wa barabara, hivyo wananchi wanapaswa kutanguliza usalama wao pale hali ya hewa inapokuwa hatarishi.
“Kama hali ya hewa ni ngumu au imekuwa na hatari, basi usitumie barabara kwa wakati huo kama kuna hatari inayosababishwa na hali ya hewa, usalama wetu kwanza na usalama wa watumiaji wengine wa barabara,” amesema.
Kwa upande wake, Faustine Matina ambaye ni mdau wa usalama barabarani amesema kampeni hiyo inalenga kuwafikia makundi yote ya watumiaji wa barabara, hususani madereva kwa kuwapa elimu kuhusu sheria, alama za barabarani na wajibu wao.
Amesema elimu hiyo itasaidia kuongeza uelewa na kupunguza malalamiko pale mtumiaji wa barabara anapochukuliwa hatua kwa kukiuka sheria, kwa kuwa atakuwa anafahamu kosa alilolifanya.
“Tumechagua kufanya kampeni hii kwa kushirikiana na Jeshi la Polisi ili kuhakikisha ujumbe unawafikia Watanzania kwamba usalama barabarani na amani Tanzania bila ajali vinawezekana, hususani katika Mkoa wetu wa Dodoma,” amesema.
Aidha, amesema kampeni hiyo imekuja wakati ambao mwisho wa mwaka unakaribia na watoto wanatarajiwa kufunga shule, hivyo elimu kwa wazazi na jamii kwa ujumla ni muhimu ili kuhakikisha watoto na wasafiri wengine wanatumia barabara kwa usalama.



0 Comments