Ticker

6/recent/ticker-posts

TUME YA HAKI ZA BINADAMU YAAHIDI KUSIMAMIA HAKI NA UTAWALA BORA

Mwenyekiti wa Tume ya Haki za Binadamu na Utawala Bora (THBUB), Wakili Dunford Mpelumbe amesema Tume hiyo itaendelea kuhakikisha Tanzania inatekeleza mikataba ya kimataifa ya haki za binadamu ambayo imesaini na kuridhia.

Wakili Mpelumbe ameyasema hayo leo Novemba 02,2026 jijini Dodoma wakati akizungumza na vyombo vya habari mara baada ya kuapishwa na Rais Samia Suluhu Hassan Ikulu Chamwino ambapo amesema serikali inaendelea kujenga mifumo madhubuti ya kisheria, kisera na kitaasisi katika sekta mbalimbali ili kuhakikisha Watanzania wanapata haki zao za kiraia, kijamii na haki nyingine zinazotambuliwa na Katiba pamoja na mikataba ya kimataifa.

"Jukumu la Tume ni kuhakikisha Tanzania kama nchi mwanachama wa mikataba hiyo, inatengeneza na kuimarisha mifumo ya kisheria, kisera na kitaasisi inayowezesha utekelezaji wa mikataba hiyo,"amesema.

Aidha, ameeleza kuwa utekelezaji wa haki za kiuchumi na kijamii unahitaji pia kutengwa kwa bajeti inayowezesha wananchi kupata huduma muhimu, ikiwemo afya na maji safi na salama.

Amesema THBUB itaendelea kutoa elimu kwa umma, kupokea na kuchunguza malalamiko ya wananchi pamoja na kusimamia misingi ya haki za binadamu na utawala bora kwa weledi na kuzingatia viwango vinavyotakiwa.

"NIkiwa pamoja na Makamu Mwenyekiti na makamishna watakaoteuliwa na Rais, tutahakikisha Tume inatekeleza majukumu yake kwa ufanisi na kuongeza hatua katika kulinda na kukuza haki za binadamu nchini,"amesema.

Katika hatua nyingine Wakili Mpelumbe amesema kuna taasisi zaidi ya 110 za kitaifa za haki za binadamu duniani zinazounda mtandao wa kimataifa wa taasisi hizo, na kwamba Tume ya Haki za Binadamu na Utawala Bora Tanzania imepata hadhi ya daraja A.

Amesema hadhi hiyo inaonyesha kuwa Tume inatekeleza majukumu yake kwa ufanisi, huku akisisitiza umuhimu wa serikali kuiwezesha Tume kwa bajeti ili iweze kutekeleza majukumu yake na kufikia wananchi wengi zaidi.







Post a Comment

0 Comments