Ticker

6/recent/ticker-posts

KATAMBI AMSHUKURU RAIS SAMIA KWA MAGEUZI MAKUBWA, TAASISI ZA WIZARA YA MAMBO YA NDANI



Na Mwandishi wetu,Dodoma

Waziri wa mambo ya ndani ya Nchi Mhe. Patrobas Katambi amemshukuru Rais wa Tanzania na Amiri Jeshi Mkuu Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan kwa mageuzi mbalimbali na uwezeshaji alioufanya kwa wizara hiyo, suala ambalo limewezesha mafanikio kadhaa ya kiutendaji ikiwa ni pamoja na kuongeza wigo wa upatikanaji wa huduma za Mahakama mtandao katika magereza 18 na hivyo kufikia magereza 84 yenye huduma hiyo kati ya magereza 129 yaliyopo Nchini.

Waziri Katambi amebainisha hayo leo Mei 25, 2026 Bungeni Mjini Dodoma wakati akiwasilisha makadirio na mapato ya Wizara ya mambo ya ndani kwa mwaka 2026/27, akisema kwamba mafanikio mengine ni pamoja na kuendelea kudumisha amani, utulivu na usalama Nchini.

Waziri Katambi ameeleza pia kuhusu kukamilika kwa mradi wa ununuzi wa mitambo na vifaa vya kuzima moto na uokoaji wenye thamani ya dola za Marekani Milioni 100, mradi ambao umewezesha upatikanaji wa mitambo 150, boti 23 na helkopta 1 kwaajili ya uzimaji wa moto na uokoaji.

"Tumenunua pia magari 3 ya kuzima moto na kemikali, magari 5 ya kubeba maji na mitambo 2 ya kuvuta magari mabovu na yaliyopata ajali. Nachukua fursa hii kumshukuru kwa dhati Rais na Amiri Jeshi Mkuu Dkt. Samia Suluhu Hassan kwa kuliwezesha Jeshi la zimamoto na uokoaji kupata vitendea kazi hivi ambavyo vitaongeza ufanisi na tija katika utendaji wa kazi." Amesema.

Akizungunzia mafanikio mengine, Waziri Katambi pia ameeleza kuhusu kufungwa kwa mifumo ya advance passengers information system (APIS) na Passenger name records (PNR) katika viwanja vya ndege vya Mwalimu Julius Nyerere na Abeid Amani Karume na Kiwanja cha ndege Mwanza, mifumo ambayo imewezesha kupatikana kwa taarifa za abiria mapema, kuzichambua na kufanya maamuzi stahiki kabla ya abiria hao kuruhusiwa kuanza safari za kuja Nchini.

Post a Comment

0 Comments