Ticker

6/recent/ticker-posts

MADEREVA 3,051,541 WACHUKULIWA SHERIA, UVUNJIFU WA SHERIA BARABARANI

 


Na Mwandishi wetu,Dodoma

Jumla ya Madereva 3,051,541 waliokiuka sheria za usalama barabarani walikamatwa na kuchukuliwa hatua za kisheria ikiwemo kuwapa onyo, kuwatoza faini, kuwafikisha Mahakamani na kuwafungia leseni katika kipindi cha Mwaka 2025/26, ikiwa ni sehemu ya Mkakati wa Wizara ya Mambo ya ndani kupitia Jeshi la Polisi katika udhibiti wa makosa ya usalama barabarani yenye kusababisha vifo na majeruhi.


Kauli hiyo imeelezwa leo Jumatatu Mei 25, 2026 na Waziri wa mambo ya ndani Mhe. Patrobas Katambi, Bungeni Mjini Dodoma wakati akiwasilisha makadirio na matumizi ya Wizara yake kwa mwaka 2026/27, akibainisha kuwa Wizara kupitia Jeshi la Polisi litaendelea na mikakati ya kusimamia ipasavyo sheria ya usalama barabarani kwa mwaka 2026/27.


"Jeshi la Polisi litaendelea na mikakati ya kusimamia ipasavyo sheria ya usalama barabarani kwa kufanya doria, kuchukua hatua stahiki kwa wanaokiuka sheria na kutoa elimu kwa umma kuhusu matumizi sahihi ya barabara." Amesisitiza Waziri Katambi.


Katika hatua nyingine, Waziri Katambi amelieleza Bunge kuhusu mchango wa Wizara kupitia Jeshi la Polisi katika operesheni za ulinzi na usalama nje ya Nchi zikihusisha ulinzi wa amani Nchini Sudan, Sudan Kusini na Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo, akisema ushiriki huo pia umeongeza ujuzi, uzoefu, weledi na nidhamu inayokidhi viwango vya Kimataifa na Kitaifa hali inayoipa sifa Tanzania.

Post a Comment

0 Comments