Na Mwandishi wetu, Dar es Salaam
Halmashauri ya Jiji la Dodoma imejipanga kujitangaza kama kitovu cha uwekezaji, biashara na maendeleo ya kisasa kutokana na kuwa na fursa nyingi kwa wawekezaji wa ndani na nje ya nchi jambo linalokuza ustawi wa wananchi na taifa kwa ujumla.
Kauli hiyo ilitolewa na Afisa Habari katika Halmashauri ya Jiji la Dodoma, Nancy Kivuyo alipokuwa akiwaelezea wananchi waliotembelea banda lao jinsi Halmashauri ya Jiji la Dodoma inavyoshiriki katika Maonesho ya 50 ya Kimataifa ya Biashara (Sabasaba) mwaka 2026 yanayofanyika katika viwanja vya Mwalimu Julius Nyerere, jijini hapa.
Kivuyo alisema kuwa Halmashauri ya Jiji la Dodoma katika kuhakikisha inavutia wawekezaji wa ndani na nje ya nchi, imeendelea kuboresha mazingira ya uwekezaji. “Mazingira ya uwekezaji yameboreshwa sambamba na mazingira ya kufanya biashara kwa kuweka mifumo rafiki inayowezesha upatikanaji wa huduma kwa urahisi na kwa wakati ili kuondoa urasimu kwa wawekezaji” alisema Kivuyo.
Akiongelea huduma zinazotolewa katika Banda la Halmashauri ya Jiji la Dodoma, alizitaja kuwa ni huduma zinazogusa wawekezaji na wafanyabiashara pamoja wananchi kwa ujumla wao. “Halmashauri ya Jiji la Dodoma katika maonesho haya inatoa huduma za ushauri na miongozo kwa wananchi na wawekezaji kuhusu upatikanaji wa maeneo ya uwekezaji na huduma za ardhi. Fursa za biashara katika sekta za kimkakati zinazokuwa kwa kasi, pamoja na taratibu za uwekezaji ndani ya jiji” alisema Kivuyo.
Nae, mkazi wa Dar es Salaam, Omary Nyange alipongeza ujio wa Halmashauri ya Jiji la Dodoma kushiriki maonesho hayo na kusema kuwa amefurahi kupata majibu ya maswali yake juu ya fursa za manunuzi ya viwanja vianvyouzwa na halmashauri. “Nitumie nafasi hii kuwapongeza ninyi kushiriki maonesho haya. Yale maswali muhimu kuhusu kununua viwanja na kuwekeza Dodoma nimeyapata na itakua rahisi sana kwangu kufanya maamuzi kwasababu sasa najua nianzie wapi” alisema Nyange.
Halmashauri ya Jiji la Dodoma inashiriki kwa mara ya kwanza katika Maonesho ya 50 ya Biashara ya Kimataifa (Sabasaba) yanayofanyika katika Viwanja vya Mwalimu Julius Nyerere, jijini Dar es Salaam, kuanzia tarehe 28 Juni hadi 13 Julai 2026 chini ya kaulimbiu isemayo “Maonesho ya Biashara ya Kimataifa Sabasaba ni Fahari ya Tanzania”.
MWISHO



0 Comments