Ticker

6/recent/ticker-posts

AMANI IKIVUNJIKA WAATHIRIKA WA KWANZA NI SISI WENYEWE, TUILINDE - DKT. MWIGULU

Na Mwandishi wetu,Mara

Waziri Mkuu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dkt. Mwigulu Lameck Nchemba, amewataka Watanzania kuendelea kulinda amani, utulivu na mshikamano akisisitiza kuwa maendeleo ya Taifa na ya mtu mmoja mmoja hayawezi kupatikana endapo nchi itakosa usalama.


Akizungumza na wananchi wa Mugumu mkoani Mara katika viwanja vya Sokoine leo Julai 1, 2026, Dkt. Mwigulu amesema wanufaika wakubwa wa amani ni wananchi wenyewe, hivyo kila Mtanzania ana wajibu wa kushiriki katika kuilinda nchi na kuepuka vitendo vinavyoweza kuhatarisha utulivu.


"Amani ikivunjika hapa muathirika wa kwanza ni wewe mwenyewe, aliyepo Iramba, aliyepi nje ya nchi yeye ataendelea na maisha yake. Ninyi hapa mkivurugana waathirika wa kwanza ni ninyi wenyewe, hilo hamuifanyii serikali wala hamumfanyii Rais wala Makamu wa Rais, mkivurugana tu hapa waathirika ni nyie wenyewe.." amesema.


Aidha, Waziri Mkuu amesema hakuna hatua ya maendeleo inayoweza kupigwa bila kuwepo kwa mazingira ya amani na usalama, akieleza kuwa wananchi wa eneo husika ndio wanaobeba athari za kwanza pindi hali ya utulivu inapovurugika, huku watu waliopo maeneo mengine wakiendelea na shughuli zao kama kawaida.


Dkt. Mwigulu ametoa wito kwa Watanzania kutekeleza wajibu wao wa kulinda Taifa, akisisitiza kuwa kila mwananchi ni mlinzi wa nchi yake. Pia amewatahadharisha wananchi dhidi ya watu wanaochochea uovu na vurugu, akidai kuwa wengi wao wapo nje ya nchi na hawana nia njema kwa Tanzania.

Post a Comment

0 Comments