Ticker

6/recent/ticker-posts

WIZARA YA KATIBA NA SHERIA YAITA WANANCHI KWENYE MAONESHO YA SABASABA


Naibu Waziri wa Wizara ya Katiba na Sheria, Zainab Katimba, amewaalika wananchi kutembelea banda la Wizara hiyo katika Maonesho ya 50 ya Kimataifa ya Biashara ya Dar es Salaam (Sabasaba) yanayoendelea jijini Dar es Salaam ili kupata huduma mbalimbali za msaada wa kisheria, elimu ya sheria pamoja na ufafanuzi wa masuala ya haki na sheria.

Akizungumza mara baada ya kutembelea banda la Wizara hiyo leo Julai Mosi, 2026, Katimba amesema ameridhishwa na namna huduma zinavyotolewa kupitia banda hilo, akibainisha kuwa Wizara pamoja na taasisi zake zinatumia maonesho hayo kuwafikia wananchi kwa kuwapatia msaada wa kisheria na ushauri kuhusu changamoto mbalimbali zinazowakabili.

Katimba amesema wananchi wenye migogoro wanapaswa kutumia fursa hiyo kupata ushauri wa kisheria na kufahamu njia bora za kutatua migogoro bila kulazimika kwenda mahakamani pale inapowezekana, akisisitiza umuhimu wa utatuzi mbadala wa migogoro katika kujenga maridhiano na mshikamano.

“Sisi tunaamini katika migogoro mbalimbali inayojitokeza njia sahihi ya kufanya ni pamoja na kutumia mbinu ya utatuzi wa Migogoro kwa njia mbadala. Tunaamini njia hii ya usuluhishi ni njia ambayo inawafanya wenye migogoro waridhiane na wote waibuke washindi tofauti na kukinzana Mahakamani ambao mmoja huibuka mshindi na anapatikana yule ambaye hajashinda.” amesema Katimba.

Banda la Wizara ya Katiba na Sheria linapatikana katika viwanja vya Sabasaba, ambapo wananchi wameendelea kuhimizwa kutembelea banda hilo ili kupata huduma mbalimbali na elimu kuhusu masuala yanayohusu utajiri asilia Kisheria

Post a Comment

0 Comments