Na Mwandishi wetu,Dar es Salaam
Amiri Jeshi Mkuu wa Majeshi ya Ulinzi na Usalama na Rais wa Tanzania Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan amesema kazi ya Jeshi la Polisi ni jukumu muhimu linalohitaji nidhamu, uadilifu, umakini pamoja na uelewa mpana wa sheria, mila na desturi za jamii.
Akizungumza leo Mei 28, 2026 akiwa mgeni rasmi katika hafla ya kuhitimisha mafunzo ya maafisa na wakaguzi wa Jeshi la Polisi iliyofanyika Chuo cha Taaluma ya Polisi Kurasini, jijini Dar es Salaam, Rais Samia amesema jukumu la kulinda watu na mali zao ni moja ya nguzo muhimu kwa ustawi wa Tanzania.
"Niwapongeze pia watanzania wenye nia njema na uzalendo kwa nchi yao kwa kuendelea kushirikiana na vyombo vyetu vya ulinzi na usalama katika kudumisha amani na utulivu wa Taifa hili. Suala la kulinda raia na mali zao ni nguzo muhimu kwa Taifa letu, bila shaka mtakubaliana nami kwamba kazi ya Polisi haiwezi kutazamwa kama kazi nyingine ya kawaida, ni kazi inayohitaji nidhamu, uadilifu, umakini na uelewa mpana wa sheria, mila na desturi na mipango ya maendeleo ya Nchi yetu." Amesema Rais Samia.
Aidha, amesisitiza umuhimu wa askari kuelewa mabadiliko ya kiuchumi na kisiasa yanayotokea duniani, akieleza matumaini yake kuwa mafunzo yaliyotolewa yataongeza tija, ufanisi na kuleta mabadiliko chanya katika utoaji wa huduma kwa jamii.

0 Comments